Psalms 64

Kuomba Ulinzi Dhidi Ya Maadui

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi)


1 aEe Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu,
uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui.

2 bUnifiche kutokana na shauri la siri la waovu,
kutokana na zile kelele za kundi la watenda mabaya.


3 cWananoa ndimi zao kama panga
na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha.

4 dHurusha mishale kutoka kwenye mavizio kwa mtu asiye na hatia,
humrushia ghafula bila woga.


5 eKila mmoja humtia moyo mwenzake
katika mipango mibaya;
huzungumza juu ya kuficha mitego yao,
nao husema, “Ni nani ataiona?”

6 Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema,
“Tumebuni mpango mkamilifu!”
Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.


7 Bali Mungu atawapiga kwa mishale,
nao ghafula wataangushwa.

8 fAtageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao
na kuwaleta kwenye maangamizi;
wote wawaonao watatikisa vichwa vyao
kwa dharau.


9 gWanadamu wote wataogopa,
watatangaza kazi za Mungu
na kutafakari yale aliyoyatenda.

10 hWenye haki na wafurahi katika Bwana,
na wakimbilie kwake;
wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!
Copyright information for SwhKC